KIKUNDI CHA UFUGAJI NYUKI CHA ‘KAZI KAZI’ TABORA CHANUFAIKA NA MATUNDA YA SEKTA YA MISITU NA NYUKI .
Na John Bera
Wafugaji wa Nyuki Mkoani Tabora wameishukuru serikali kwa kuwasaidia kwa hali na mali katika ufugaji wa nyuki hatua ambayo imechochea Vijana wengi kujiingizia kipato kupitia sekta hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Kikundi cha Kazi Kazi kinachojihusisha na ufugaji nyuki mkoani humo, Halima Bedui amesema anaishukuru Serikali kupitia TFS kwa kuwapa miti 4000 pamoja na kuwapatia mafunzo ya ufugaji nyuki ambapo mafunzo hayo yaliwahamasisha kuchangishana na hadi sasa wameweza kujipatia mizinga 30 ya nyuki inayowasaidia kuzalisha zaidi ya kilo 15 za Asali kwa kila mzinga kila mwaka.
Bedui amesema Kikundi hicho cha Kazi kazi kimezaliwa kutoka kwenye kikundi cha Mzinga wa Mama Samia ambacho pia kinajihusisha na shughuli za Ufugaji nyuki.
Ameongeza kuwa kutokana na mafunzo waliyopewa wanachaka asali kwa kufuata taratibu za kukidhi viwango vya ubora.
“Huwa tunatengeneza juisi ya ntonga, tunasindika sabuni za asili za ntonga, tuna vitu vingi, lengo na dhumuni ni kuvuna mazao mengi ya nyuki ambayo tutayatumia kwakuwa tunapoenda kwenye Maonesho ya Biashara yanauliziwa Tunaishukuru Serikali yetu inatusaidia Kikundi chetu kimekwenda Uganda na Burundi kupeleka asali kwa msaada wa serikali” amesema Bedui.
Aidha, Bedui ameeleza kuwa asali ya Tabora haina Tumbaku kama ambavyo baadhi ya watu wanaitilia mashaka pindi wanapoenda kwenye Maonesho mbalimbali na hivyo kusisitiza watu wajitokeze kwa wingi kununua Asali hiyo kwasababu ni bora.
“nyuki hawali sumu, huku Tabora tunalima alizeti, mbogamboga kama vile majani ya maboga ambapo nyuki wanakimbilia sana kwenye maua kuliko kwenye tumbaku, asali yetu ya Tabora ilishika namba mbili Kwa ubora “-Amefafanua Bedui.
Kwa upande wake mwana kikundi ambaye pia ni kijana kutoka kikundi hicho, Albert Nkuba kwa niaba ya wenzake ametoa rai kwa Vijana wa Kitanzania kutunza rasilimali za misitu ikiwa ni pamoja na kupanda miti na kuilinda ikiwemo miti ya asili kama Wazee wa karne hiyo walivyofanya na kizazi cha sasa kinanufaika nayo hivyo waitunze kwa kizazi kijacho badala ya kufanya uharibifu katika mazingira.