November 15, 2024

Makamu waRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt .Philipo Mpango ametoa siku 90

0

 Na WMJJWM, Dodoma

Makamu waRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt .Philipo Mpango  ametoa siku 90 kwa wamiliki wa makao ya watoto na vituo vya malezi ya watoto wadogo mchana kuhakikisha wanasajili vituo hivyo na kufuata taratibu zote za uendeshaji wa vituo hivyo.


Mhe. Dkt. Mpango ametoa agizo hilo kupitia hotuba yake iliyowasilishwa kwa niaba yake na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dotto Biteko  wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Maafisa Ustawi wa Jamii jijini Dodoma leo Septemba 6, 2023.


“Naelekeza Waziri mwenye dhamana kushirikiana na vyombo vya sheria ili kuwabaini wamiliki hao na kuwachukulia hatua za kisheria. Baada ya hapo, ukaguzi wa kina utafanyika ili kuwabaini watakaoshindwa kutimiza vigezo vya kisheria ili wachukuliwe hatua.” amesema Dkt. Biteko.


Ameongeza kuwa kada ya Ustawi wa Jamii ni muhimu katika maendeleo ya Taifa na amewataka 


Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya huduma za Ustawi wa Jamii kwa mujibu wa mwongozo wa mipango, bajeti na taarifa za Ustawi wa Jamii.


Aidha, Mhe. Biteko amesisitiza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuendelea kutoa ajira kwa maafisa Ustawi wa Jamii ili kusaidia kutoa huduma bora za Ustawi wa Jamii.


Awali, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akimkaribisha Mhe. Biteko, amesema huduma za ustawi wa jamii zinalenga kusaidia na kuwezesha makundi maalum kushiriki shughuli za maendeleo na kuisaidia jamii kuwa salama kwa kuwa na afua za kuzuia changamoto zinazoweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo uhalifu. 


“Katika kuboresha huduma za Ustawi wa jamii nchini Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuandaa nyenzo muhimu za utekelezaji wa huduma za ustawi pamoja na kupunguza changamoto ya upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii takribani 20,057 sawa na asilimia 95.3 ya wanaotakiwa kuanzia ngazi ya mkoa hadi Kijiji/Mtaa.” amesema Mhe. Gwajima.


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Toufiq ameiomba Serikali kutimiza ahadi ya kuajiri Maafisa Ustawi wa Jamii ili kutatua changamoto ya upungufu wa Maafisa hao na kukidhi mahitaji.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Seif Shekalaghe amesema lengo la mkutano huo ulifanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2019 ni kujadili afua na changamoto za utekelezaji wa majukumu ya Maafisa Maendeleo ya Jamii, kufanya tathmini, kubadilishana uzoefu na kuja na namna bora ya kuimarisha sekta hiyo kwa manufaa ya wananchi.


Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Ustawi wa Jamii, Mwenyekiti wa Maafisa Ustawi nchini Martin Chuwa amesema jukumu kubwa la Ustawi wa Jamii ni kufanya utambuzi, tathmini na kutoa huduma, Aidha kuanzishwa kwa Wizara inayoratibu utendaji wa Ustawi wa Jamii, ahadi ya kuajiri Maafisa Ustawi wa Jamii itapunguza changamoto ya upungufu mpango kwenye halmashauri.



Mkutano huo unakwenda sambamba na Uzinduzi wa maadhimisho ya Miaka 50 ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Uzinduzi wa Wiki ya Ustawi wa Jamii pamoja na Uzinduzi wa Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji, Usimamizi na Uratibu wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa 2023; Mwongozo wa Mafunzo ya Uwiano wa Kijinsia na Ujumuishwaji Jamii katika Huduma za Ustawi wa Jamii 2022; na Kiongozi cha Taifa cha Uelimishaji wa Huduma za Ustawi wa Jamii na Majukumu ya Viongozi 2022.




Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page