November 15, 2024

Wizara Ya Maliasili Na Utalii Yaendelea Kuwajengea Uwezo Viongozi Wa Jumuiya Za Uhifadhi Kusimamia Rasilimali Za Wanyamapori

0

 Na Mwandishi Wetu, Singida,


WIZARA  ya Maliasili na Utalii imeendelea kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini kwa kutoa mafunzo maalumu kwa viongozi wa Jumuiya za Uhifadhi wa Wanyamapori (WMAs) katika wilaya ya Waga, Mkoani Singida, na Chamwino Jijini Dodoma. 

Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo muhimu yanalenga kuwajengea viongozi hao uelewa wa pamoja juu ya umuhimu wa  kusimamia rasilimali za wanyamapori, hasa katika maeneo ambayo wananchi wametenga maeneo yao kwa ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi.


Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika mkoani Singida, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Rose Mdendemi amesema mafunzo hayo yamejikita kuwapa viongozi hao uwezo mpana wa kuendeleza shughuli za uhifadhi kwa uweledi, ikiwa ni pamoja na kusimamia rasilimali katika maeneo  ya Jumuiya hizo.

Mafunzo hayo yamewezeshwa na Mradi wa Kudhibiti Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara (IWT – PROJECT).


Mradi huo endelevu  unatekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na unalenga kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu  katika shughuli za uhifadhi nchini, kudhibiti ujangili,  kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu, pamoja na kuhakikisha wananchi wananufaika kupitia shughuli za utalii.

“ Kwa kifupi tunaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan hasa katika kuendeleza utalii kwa kuwapatia wananchi uelewa na ujuzi wa namna bora ya kusimamia maeneo yao ya hifadhi na  kupunguza migongano  baina ya binadamu na wanyamapori wakali na wabaribifu ” amesema.


Aidha, amelishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa  Mataifa (UNDP),  kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwa Wizara katika kutekeleza majukumu hayo.

 “Tunaamini mafunzo haya yatawezesha wananchi kusimamia rasilimali hizi vizuri na hatimaye kufikia malengo ya kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.”

Kwa upande wake, Rachel John, Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka wilaya ya Mufindi Pamoja na Afisa Wanyamapori Mkuu wa Wilaya ya Chamwino mkoa wa Dodoma, Yusuph Nyonyi, wameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo ambayo ni muhimu katika jamii zilizotoa maeneo yao kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.

Naye Mwakilishi Kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa  Mataifa (UNDP), Damas Masologo amesema nimatarajio ya Shirika hilo kuwa Mradi utapokuwa umekamilika, Jumuiya mbalimbali za Wanyamapori nchini zitakuwa zimesimama vizuri  hasa katika kutekeleza majukumu yao.



Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page