November 15, 2024

Rais Dkt. Samia Azitaka Posta Za Afrika Kujiendesha KIDIJITALI

0

Na Mwandishi Wetu,

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezitaka Posta Barani Afrika kwenda na wakati katika utendaji wake kwa kutumia mifumo ya kidijitali lengo ikiwa kuendana na wakati pamoja na mahitaji ya soko ili kujenga umuhimu wa uwepo wa Posta katika kuwahudumia waafrika.

Ameyasema hayo leo tarehe 02 Septemba, 2023 wakati alipokuwa akizindua rasmi Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU TOWER), Jijini Arusha.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mhe. Rais ameeleza kuwa Posta haiwezi kubaki kama ilivyokuwa miaka ya nyuma bali ijikite katika kuboresha mifumo yake ili kurahisisha huduma kwa jamii na jengo hili la Makao Makuu likawe chachu ya mabadiliko kuongeza ubunifu, kujengeana uwezo na kufanya mageuzi ya utendaji baina ya nchi wanachama PAPU.

Aidha, Dkt. Samia ameongeza kuwa, jengo hili likalete uwiano wa maendeleo ya Posta za Afrika ili ziweze kutoa huduma zinazoweza kutegemewa na jamii na kwa kufanya hivyo itaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali na posta kuendelea kuleta tija.

Katika hatua nyingine Mhe. Rais Dkt. Samia amezindua Stempu za nchi mbalimbali Afrika ikiwemo Algeria, Misri, Moroco, Nigeria, Senegal na Zimbabwe zenye picha ya jengo la PAPU pamoja na vivutio vya nchi hizo ikiwa ni sehemu ya kuitangaza Afrika duniani huku akitumia nafasi hiyo kuzipongeza nchi hizo pamoja na Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kwa kutumia fursa hiyo kujitangaza kimataifa.

1000250442

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuimarisha huduma za Posta katika Bara la Afrika kunaweza kuikomboa Afrika kiuchumi na kuchochea maendeleo huku akisisitiza mshikamano kwa bara la Afrika ili kuendelea kuikomboa Afrika kiuchumi.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Dkt. Sifundo Chief Moyo amesema kuwa Sekta ya Posta Afrika imekuwa sekta muhimu katika kuchangia mabadiliko ya kidijitali katika jamii na Jengo la PAPU linatazamiwa kuwa kituo cha mabadiliko ya kidijitali na uratibu wa maendeleo ya Sekta ya Posta katika Bara la Afrika.

1000250440

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page