Ofisi ya DPP Wakutana Menejimenti Na Watendaji Kuweka Mikakati Ya Kazi
Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amefungua Kikao kazi baina ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Menejimenti, Wakuu wa Mashtaka wa Mkoa, Wilaya, Waendesha Mashtaka Viongozi (PAI), Wahasibu/ Watendaji wanaofanya kazi za kihasibu katika Mikoa na Wanachama hai wa Mashtaka SACCOS kinachofanyika tarehe 28 hadi 29 Agosti, 2023 Jijini Dodoma.
Akifungua kikao kazi hicho Mkurugenzi Mwakitalu ameeleza kuwa lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali yanayofanywa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kupima utendaji bora wa kazi.
Sambamba na hayo, Mkurugenzi Mwakitalu amesema kuwa katika kikao kazi hicho watajadiliana na kukumbushana masuala mbalimbali zikiwemo changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ili kutoa mapendekezo ya kuzitatua kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa Taasisi.
Pia Mkurugenzi Mwakitalu amewataka Viongozi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha watumishi wengine waliopo chini yao ambao bado hawajajiunga na Mashtaka SACCOS ili waweze kujiunga na Chama hicho.
“Tujiunge na tukope kwenye SACCOS yetu kwa riba nafuu, masharti nafuu ili tuweze kupunguza changamoto za kifedha tunazokutana nazo.” Ameyasema hayo Mkurugenzi Mwakitalu.