Mtume Mwamposa Aanza Kumwaga Televisheni Za Bure Kwenye Magereza
Na Mwandishi Wetu
Mhubiri maarufu wa Kikristo nchini, Mtume Boniface Mwamposa ametoa msaada wa Televisheni tatu za kisasa kwa Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam.
Televisheni hizo zimetolewa kupitia huduma maarufu inayoongozwa na Mtume Mwamposa ya ‘Arise and Shine’ ( Amka Uangaze), kwa lengo la kuwapa fursa wafungwa ndani ya gereza hilo kupata taarifa zinazohusu masuala mbalimbali yanayoendelea nchini, na nje ya nchi.
Akizungumza leo (Jumapili) wakati akihubiri katika ibada ya kwanza kwenye viwanja vya Tanganyika Parkers, Mtumishi huyo wa Mungu, maarufu kwa jina la ‘Bulldozer’, amesema mipango iko mbioni kugawa Televisheni kwenye magereza yote nchini Tanzania.
Aliongeza kuwa, maono ya jumla ya msaada huo ni kuwapa wafungwa nafasi adhimu ya kutazama na kushiriki katika mafunzo ya kiroho, ibada, na huduma za maombezi ambazo zinarushwa kupitia vipindi na chaneli mbalimbali za Televisheni, ikiwemo Arise and Shine.
“Vipindi vya mafundisho ya neno la Mungu na maombi ambayo vinarushwa hewani kupitia TV ni vya muhimu sana katika kusaidia kuwakomboa wafungwa kutoka kwenye minyororo ya roho chafu na hivyo kuwasaidia kujiepusha na kujihusisha na matendo maovu,” Bulldozer alisema.
Amesema kuwa wiki ijayo, matarajio ni kupeleka Televisheni katika magereza ya Mkoa wa Tabora, na baada ya hapo, mpango huo unaoendela katika mikoa mingine.
Huduma ya Arise and Shine, yenye makao yake makuu katika eneo la Tanganyika Parkers, jijini Dar es Salaam, chini ya uongozi wa Mtume Mwamposa, imekuwa huduma ya kiroho yenye kuvutia mamia na maelfu ya waumini kutoka mataifa mbalimbali duniani.