November 15, 2024

Milki 60,000 Kusajiliwa Kigoma Na Chalinze

0

 

Na Mwandishi wetu
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi imejipanga kusajili milki takribani 60,000 ambapo Manispaa ya Kigoma Ujiji milki 10,000 zitasajiliwa na katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze milki 50,000 zitasajiliwa.


Hayo yalisemwa na Meneja wa Urasimishaji Mijini Bw. Leons Mwenda wakati wa zoezi la uhakiki wa taarifa za umiliki wa vipande vya ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani tarehe 26/08/2023.

Bw. Mwenda alisema kuwa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji makadirio ya makazi holela ni takribani 10,000 na ifikapo Disemba 2023 makazi hayo yote yatakuwa yamesajiliwa na kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze takribani Milki 20,000 zinatarajiwa kusajiliwa ifikapo Disemba 2023 kati ya milki 50,000 ambapo milki 30,000 zinatajiwa kutambuliwa, kupangwa na kupimwa na Makampuni binafsi ya upangaji na upimaji. 

Bw. Mwenda alisema ‘‘Wizara ya ardhi kwa kupitia Mradi huu imedhamiria kutambua maeneo hayo ili kuboresha hali ya makazi nchini kwa kupanga miundo mbinu ya barabara, matumizi ya ardhi na kuboresha usalama wa milki kwa kutumia mifumo na utoaji wa hati miliki kwa wananchi kwa kuzingatia haki za umiliki wa ardhi kwa makundi maalum kama vile wafugaji na wakulima, wanawake, vijana, walemavu, wazee na watoto’’.

‘‘Kati ya Mwezi Julai 2023 hadi Agosti 2023 zaidi ya makazi 3,000 (Manispaa ya Kigoma Ujiji) na makazi 5,000 (Halmashauri ya Chalinze) yametambuliwa na kupangwa. Kazi ya uhakiki wa taarifa za umiliki katika Kata za Kibirizi (Kigoma) na Pera (Chalinze) inaendelea’’ aliongezea Mwenda.

Wakati wa zoezi hilo la uhakiki wa taarifa likiendelea katika Mtaa wa Kibirizi, Kata ya Kibirizi (Manispaa ya Kigoma Ujiji) na Mtaa wa Pera Kata ya Pera Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Maafisa mipango Miji wanaosimamia kazi hizi kwa Manispaa ya Kigoma Bw. Oden Martin na Deo Msilu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze wamewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kuhakiki taarifa hizo kuona usahihi wa majina yao, namba za NIDA, namba za simu, matumizi ya ardhi na aina ya umiliki. Wakati wa zoezi hilo, wananchi wameombwa kutoa taarifa ikiwa kuna mmiliki ameomba kujimilikisha kipande cha ardhi ambacho sio chake

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi ni mradi unatekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa muda wa miaka mitano (2022/2027) ukiwa na lengo la kutambua, kupanga na kupima makazi 1,000,000 na kutoa leseni za makazi 1,000,000 katika Halmashauri 34 Nchini kwa upande wa mijini. Ili kufanikisha malengo tajwa, kazi zitafanyika kwa kutumia vikosi kazi vya watumishi wa Serikali na Makampuni binafsi ya Upangaji na upimaji. Kwa sasa timu za watumishi wa Serikali zinaendelea na utekelezaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Manispaa ya Kigoma Ujiji na Wilaya ya Chalinze. Timu za watumishi wa Serikali zinatararija kuendelea na mpango kazi katika Halmashauri za Manispaa ya Tabora na Kahama na Halmashauri ya Wilaya ya Nzega.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page