HAMASISHENI WANANCHI KUJIUNGA NA VYAMA VYA USHIRIKA – DC SHEKIMWERI
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Jabir Shekimweri, ametoa wito kwa Wanachama Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kuhakikisha kuwa wanahamasisha wananchi kujiunga na Vyama vya Ushirika ili kuweza kunufaika miradi mbalimbali inayosimamiwa na Sekta ya Ushirika nchini ukiwepo Mradi wa Matumizi safi ya nishati safi ya kupikia inayosimamiwa na Shirika la Maendeleo la Uholanzi ( SNV).
Mhe. Shekimweri ametoa wito huo leo Agosti 27, 2024 wakati wa Uzinduzi wa awamu ya pili ya Program ya kukuza mtaji kupitia mzunguko wa mauzo ya majiko ya Umeme kwa wanachama wa SACCOS wa Mikoa ya Dodoma, Dar es salaam, Morogoro, Arusha, Pwani, Njombe na Mwanza uliofanyika Jijini Dodoma.
“Nitoe wito kwa TCDC na Wanachama wa SACCOS, kuendelea kuhamasisha Wananchi kujiunga na Vyama vya Ushirika ili kunufaika na mradi huu; Ushirikiano huu umekuwa sehemu muhimu sana katika kukuza maendeleo ya Ushirika hususan katika matumizi ya teknolojia safi ya kupikia ikiwa na nia ya utunzaji wa mazingira,” amesema Mhe. Shekimweri.
Naye Naibu Mrajis – Udhibiti, Collins Nyakunga, ametoa rai kwa Vyama vya Akiba na Mikopo kuendelea kupanua huduma zao na kutoa huduma za kifedha kwa Wanachama wao kwa njia rahisi na yenye faida.
“Katika uzinduzi wa Program hii, tunashukuru wenzetu wa SNV kwa kuweza kufanikisha program hii ya kipekee inayohusiana na kukuza mtaji kupitia mzunguko wa mauzo wa majiko ya umeme,” amesema Nyakunga.
Amesema kuwa hiyo ni fursa ya kipekee kwa Vyama vya Akiba na Mikopo kutoa msaada wa kifedha kwa Wanachama kwa njia rahisi na yenye faida, kwa kuwa SACCOS shughuli yake kubwa ni kuzungusha fedha ili ilete faida.
Kaimu Mkurugenzi wa SNV, Ramadhani Mshindo, amesema malengo ya Program hii ni kutoa fursa muhimu kwa Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kuweza kupanua huduma zao na kutoa msaada wa kifedha kwa Wanachama kwa njia rahisi na yenye faida ambapo Vyama vya Ushirika vitapatiwa majiko ya awali kwa ruzuku kwa lengo la kuhamasisha wanachama watumie majiko ya umeme.
Ameongeza kuwa; Vyama vya Ushirika vitapatiwa motisha kwa kila jiko vitakavyouza na kuwakopesha Wanachachama wake.
Programu hii inalenga kuwafikia watumiaji 3,000 wa majiko ya umeme ifikapo mwezi Juni, 2025 na SNV inatarajia kushirikiana na SACCOS 12 kwa kuanzia, ambapo SACCOS 22 zitashindanishwa,na Vyama vya Ushirika vitapatiwa majiko ya awali kwa ruzuku, kwa lengo la kuanza kuhamasisha wanachama wake kutumia majiko hayo na pia vyama vitapatiwa motisha kwa kila jiko vitakavyouza au kuwakopesha wanachama wake.