WANAFUNZI MSALATO NA BUIGIRI WAPEWA ELIMU YA AFYA KUHUSU MATUMIZI SAHIHI YA TAULO ZA KIKE NA HEDHI SALAMA
.
Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Wizara ya Afya imetoa elimu ya afya kuhusu matumizi sahihi ya taulo za kike na hedhi salama kwa wanafunzi wa kike kutoka shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato pamoja na shule ya Msingi ya mwenye mahitaji maalum Buigiri Mkoani Dodoma.
Akitoa elimu hiyo wakati wa zoezi la kukabidhi taulo za kike 1200 kwa shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato, na taulo 480 kwa shule ya Msingi wenye mahitaji maalum Buigiri Mkoani Dodoma,Bi. Mariam Mashimba kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ndogo ya Afya Mazingira amesema matumizi ya taulo za kike muda mrefu kunaweza kusababisha maambukizi kwenye via vya uzazi.
“Msitumie muda mwingi na kusababisha maambukizi kwenye via vya uzazi na ukishatumia unatakiwa kuweka mahali sahihi kwa ajili ya kuchomwa sio kutupa ovyo kwenye matundu ya vyoo”amesema Mariam.
Kwa upande wao Mwalimu Mkuu Shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato Mwasiti Bahati Msokola pamoja na mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya wenye mahitaji maalum Buigiri wamesem taulo hizo za kike zitasaidia kwa wananfunzi wa kike na kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule hizo wametumia fursa hiyo kuipongeza serikali kwa kushirikina na Halotel kwa msaada huo.
Elimu ya afya kuhusu tahadhari ya ugonjwa wa Mpox nayo haikuachwa nyuma ambapo Beauty Mwambebule kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma ametoa wito kwa wanafunzi kuwa na desturi ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka misongamano.