KAMISHNA WAKULYAMBA ASISITIZA MATUMIZI YA SHERIA NA KANUNI KATIKA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA UHIFADHI
Na.Joyce Ndunguru, Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba asisitiza matumizi ya sheria na kanuni katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za uhifadhi.
Kamishna Wakulyamba ameyasema hayo
leo Septemba 1, 2024 wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika ofisi za Makao Makuu ya TAWA yaliyopo Mkoani Morogoro kwa lengo la kuongea na watumishi ili kuimarisha utendaji kazi pamoja na kukagua maeneo ya kazi.
“Kama wahifadhi tunapaswa kufahamu sheria zote zinazosimamia masuala ya uhifadhi zilizopo katika Taasisi zetu pamoja na za Taasisi zingine za uhifadhi zilizopo ndani ya Wizara ya Maliasili na utalii” amesema Kamishna Wakulyamba.
“Pamoja na kufahamu sheria na kanuni zilizopo ndani ya Wizara yetu, ni vyema kufahamu na kuzingatia sheria nyingine za Nchi ambazo zinatuzunguka ili ziweze kutusaidia katika utekelezaji wa majukumu yetu mfano sheria inayohusiana na ukusanyaji wa vielelezo kuanzia kwenye ukamataji hadi kuwasilishwa mahakamani” ameongeza Kamishna Wakulyamba.
Sambamba na hilo, Kamishna Wakulyamba amewapongeza Askari kwa kazi nzuri wanazofanya na amewaasa kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu.
Awali, Kaimu Naibu Kamishna anayeshughulikia huduma za uhifadhi, Mlage Kabange alitoa taarifa kuhusu
masuala mbalimbali yanayosimamiwa na TAWA huku akibainisha mafanikio na changamoto ya wanyama wakali na waharibifu hususan katika Mikoa ya Kusini mwa Tanzania.
Katika ziara hii ya kikazi, Kamishna Wakulyamba aliambatana na Maafisa kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi , Mrakibu wa Polisi Joseph Jingu na Mrakibu wa Polisi Ocsar Felician waliopata fursa ya kutoa mafunzo maalum kwa watumishi wa TAWA.