WAZIRI MKUU MAJALIWA AFUNGUA SEMINA ELEKEZI YA VIONGOZI WAANDAMIZI WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuzingatia 4 R za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo ni Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na kujenga upya taifa katika kutekeleza jukumu la kuimarisha usalama wa raia na mali zao hivyo kuifanya Tanzania kuendelea kuwa na amani na usalama.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo Septemba 06, 2024 wakati akifungua Semina Elekezi kwa Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inayofanyika mkoani Kilimanjaro.
‘Wizara mnatambua kuwa Mhe. Rais ametambulisha falsafa ambayo imetusaidia kuendesha Nchi na falsafa hii inagusa maeneo ya maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya Taifa, hivyo nitoe wito kwa Vyombo vyote vya Usalama vilivyo chini ya Wizara hii kuzingatia maeneo haya manne wakati wote mnapotekeleza majukumu yenu”
Alisema kwa kuzingatia falsafa hiyo ambayo ni muhimu katika ustawi wa Nchi yetu kila mmoja akitekeleza wajibu wake Tanzania itaendelea kuwa salama.
Aidha, ameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na vyombo vyake vyote kuhakikisha kuwa wanaendelea kutekeleza maelekezo ya Tume ya Haki Jinai ili kulinda haki za binadamu kwa kuwa ni msingi wa Utawala Bora na Usalama wa Taifa.
Alisema, Serikali imejielekeza katika kutoa huduma bora kwa kuanzisha maboresho katika Taasisi za Haki Jinai, hivyo Wizara na Vyombo vyote vihakikishe kuwa, vinatekeleza mapendekezo hayo ili kuendelea kutoa haki kwa usahihi.
Vile vile amesisitiza Vyombo vya Usalama hususani Polisi na Magereza kutumia nishati safi ambazo ni gesi, umeme na makaa ya mawe ili kuendelea kulinda mazingira.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema kuwa, pamoja na mafanikio makubwa waliyoyapata, Wizara inaendelea kufanyia kazi maelelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanyia maboresho hususani maelekezo ya Tume ya Haki Jinai ndiyo maana Wizara pamoja na watendaji wengine wamekutana ili kujengeana uwezo wa kusimamia maelekezo hayo.