TAEC YAFUNGUA DIRISHA LA MAOMBI YA NAFASI ZA UFADHILI WA SAMIA EXTENDED
SERIKALI, kupitia Tume ya Nguvu ya Atomu Tanzania (TAEC) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefungua rasmi dirisha kwa waombaji wenye sifa za kuomba nafasi za kusomea Shahada ya Juu ya Teknolojia ya Sayansi ya Nyuklia kupitia ufadhili wa Samia Scholarship Extended (SSE) 2024/25.
Katika mwaka fedha 2024/25,Serikali ilitenga jumla ya Shilingi bilioni 1.6 ili kuiwezesha TAEC kufadhili wanafunzi watano kwenda nje ya nchi kusoma Shahada ya Uzamili katika fani mbalimbali zinazohusiana na teknolojia ya Nyuklia.
Akitangaza juu ya kufunguliwa kwa dirisha la kuomba nafasi hizo muhimu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda alisema ufadhili huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuongeza idadi ya wataalamu wa sekta ya sayansi ya mionzi hapa nchini.
“Tangu mwaka wa fedha 2022/23, Serikali kupitia Wizara ya Elimu ilianza programu ya kutoa ufadhili kwa asilimia 100 kwa wanafunzi bora katika masomo ya sayansi kuanzia ngazi ya kidato Cha sita,” alisema.
Amesema ufadhili huo unawalenga wanafunzi wenye sifa ambao wamechagua kufanya shahada ya kwanza katika masomo ya Sayansi, Habari na Teknolojia (IT), Uhandisi na Hisabati, pamoja na Elimu Tiba.
“Utafiti hadi sasa umebaini kuwa Tanzania inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wataalam katika sekta ya sayansi ya nyuklia, hivyo kulazimu serikali kuja na mpango madhubuti wa kusaidia kupunguza nakisi hiyo,” alisema.
“Kwa mfano” Waziri Mkenda alieleza, “Tanzania kuna wataalam sita tu wa Medical Physics pamoja na Nuclear Medical Doctors,” alizindua.
Na aliongeza, nchi ina mtaalamu mmoja tu wa Radiochemistry, na Madaktari wawili tu wa Radiopharmacists.
“Uhitaji wa teknolojia ya sayansi ya nyuklia nchini Tanzania unaendelea kuongezeka kwa kasi kila siku kwa hivyo, lazima tutengeneze idadi kubwa ya wataalam wa hali ya juu,” Prof Mkenda alisisitiza.
Akitoa maelezo juu ya utaratibu uliowekwa wa kuomba nafasi za ufadhili huo, Mkurugenzi Mkuu (DG) wa Tume ya Nguvu ya Atomiki Tanzania (TAEC), Prof Najat Kassim Mohammed, alieleza kuwa waombaji wenye sifa wanapaswa kujaza fomu husika zinazopatikana kupitia tovuti ya TAEC.
Hata hivyo, Pro Najat amesema waombaji pia wanaweza kupata fomu hizo kupitia tovuti ya Wizara ya Elimu.
“Ufadhili huu utawanufaisha wanafunzi (wataalamu) wanaotaka kusoma maeneo angalau matano yanayohusu sayansi na teknolojia ya nyukilia,
Aidha, Prof Najat amesema waombaji wanatakiwa kuomba kusoma katika Vyuo vinavyosimamia udhamini huo ni vile vinavyotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), katika nchi kadhaa, zikiwemo Australia, Canada, China, Ufaransa, India, Finland na Korea Kusini. miongoni mwa wengine.
TAEC ni taasisi yenye dhamana ya udhibiti wa matumizi salama ya mionzi nchini na uhamasishaji wa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini ambapo Taasisi hii iko chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.