November 14, 2024

MAMENEJA WA MIKOA WA TARURA WATAKIWA KUTENGA BAJETI ZA MATENGENEZO YA TAA ZA BARABARANI

0

 

Mtwara

Mameneja wa Mikoa wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) nchini wametakiwa kutenga bajeti za matengenezo ya taa za barabarani ili kuhakikisha zinatengenezwa pindi taa hizo zinapoharibika.

Agizo hilo limetolewa na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff wakati wa kikao kazi na Watumishi wa TARURA Mkoa wa Mtwara kilichofanyika leo tarehe 11.11.2024 katika Ofisi ya Meneja wa TARURA Mkoa wa Mtwara.

Mhandisi Seff amesema kwamba Mameneja wa TARURA wa Mikoa yote Nchini wanapaswa kutenga fedha za ukarabati wa taa kwenye bajeti zao za kila mwaka ili wananchi waweze kutumia barabara hizo wakati wote hususan usiku kwa shughuli za kiuchumi na kuongeza usalama wa watembea kwa miguu.

Mhandisi Seff yupo katika ziara ya kikazi Mkoani Mtwara ambapo baaada ya kuongea na Watumishi wa TARURA-Mkoa alitembelea barabara za lami za ukanda wa viwanda za EPZA zilizojengwa na TARURA mwaka 2021 zenye urefu wa kilometa 1.3 zilizopo Mtwara Mjini.

Katika barabara za ukanda wa EPZA Mtendaji Mkuu amemtaka Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Mtwara kuzifanyia matengenezo ya mara kwa mara barabara hizo ikiwemo kufyeka nyasi ili kuzilinda zisiharibike na ziweze kudumu kwa muda mrefu kama ilivyokusudiwa.

Barabara za Ukanda wa Viwanda EPZA zimekuwa na tija kubwa kiuchumi kwa kuongeza kasi ya ukuaji wa shughuli za viwanda katika Mkoa wa Mtwara na kuongeza ajira ikiwa ni Utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala cha Mapundizi CCM ya mwaka 2020/2025.

Naye, Meneja wa TARURA Mkoa wa Mtwara Mhandisi Zuena Mvungi amesema kuwa wamepokea maelelezo yote na ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote ikiwemo ya kutenga fedha za kukarabati taa za barabarani kwenye bajeti zao ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuzitumia barabara hizo wakati wote na kwa usalama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page