November 14, 2024

ACHENI KUFOKEA FOKEA WATUMISHI WENZENU:WAZIRI SIMBACHAWENE

0

 

Na. Lusungu Helela

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George  Simbachawene ameonesha kukerwa na  baadhi ya Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi za Serikali  wenye  tabia ya kuwafokea Watumishi  walio chini yao  wakiamini kufanya hivyo ndio uongozi.

Amesema baadhi yao hudiriki hata kuwatukana watumishi huku akisisitiza jambo hilo ni kosa kubwa na kama kuna Kiongozi anataka kufanya ufanisi lakini anafikia hatua ya kutukana watumishi huyo hafai kabisa kwani zipo kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa umma za kuchukua kama mambo hayaendi sawa

Ametoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma katika Kampasi ya Dar es Salaam ambapo amesema hivi vitu ni maslahi ya umma, Kiongozi makini hahitaji kununa wala kufokafoka cha msingi ni kuchukua hatua.

” Kuna watu walikuwa wanasoma  bidii zote ili wapate nafasi kwenye utumishi wa umma ili waje wakomeshe watu, kuna watu kazi yao kubwa ni kuwashughulikia watu na hiyo ndo raha yao” ameng’aka Simbachawene

Amesema mshahara hata uwe mkubwa kiasi gani kwa watumishi kama mahali hapo  pa kazi hakuna amani, kuna manyanyaso, hakuna kuthaminiwa na kutambuliwa kwa mchango wao hapawezi kuwa na ufanisi wa kazi.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Simbachawene amesema akitaka Chuo Cha Utumishi wa Umma kisisubiri kuitwa kitoe mafunzo ya kujengeana uwezo mahali pa kazi pamoja na kuhakikisha  kinatoa mafunzo ya awali kwa watumishi wanapoanza kazi  ili waweze kutambua haki na wajibu wao.

Amesema huko kwenye Taasisi za Serikali kuna shida kubwa ya migogoro ya watumishi isiyoisha ilhali Chuo cha Utumishi kipo ” nilitegemea kuona mnafika kwenye Taasisi hizo  kwa lengo la kutoa mafunzo kwa watumishi ili mambo yaende lakini hamfanyi hivyo”

” Nakutana na mashirika makubwa ya nje yananiomba yakatoe mafunzo ya kuwajengea uwezo katika Taasisi fulani za Serikali wanaona mambo hayaendi sawa ilhali ninyi mpo hii sio sawa  changamkeni mna fursa nyingi za kubadilisha utumishi wa  umma nchini.

Amesema Chuo hicho kifanye mafunzo ili kuepuka watumishi wengi kupelekana mahakamani au TAKUKURU ilhali Chuo cha Utumishi kupitia mafunzo ya kujengeana yangetolewa ingekuwa ni mwarobaini na  hali  isingefikia huko.

Awali Mkuu wa Chuo hicho, Dkt.Mabonesho ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mchango  mkubwa wa kutatua tatizo la watumishi katika Chuo ambacho kilikuwa kinakabiliwa na uhaba wa watumishi na hivyo kukwamisha kufikia malengo waliyojiwekea

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George  Simbachawene akizungummza na  Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma  Kampasi ya Dar es Salaam

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page