Balozi Polepole Kumwaga Fursa Tatu Za Kiuchumi Kutoka Cuba
Na Mwandishi Wetu
BALOZI wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Herson Polepole ametangaza kuleta neema ya fursa tatu kubwa za kiuchumi nchini Tanzania.
Akizungumza kutoka Jiji la Havana, Makao Makuu ya Cuba, mwanadiplomasia huyo kijana amewataka watanzania wote, hususan vijana, kukaa mkao wa kupokea na kuhakikisha wanazitumia fursa hizo tarajiwa ili kujikwamua kiuchumi, lakini pia, kuchochea maendeleo ya nchi kwa ujumla.
“Helo wataalam wenzangu, mambo vipi? Habari za nyumbani Tanzania, bila shaka mpo vizuri, napenda kuwajulisha kuwa Mungu akipenda ndani ya wiki mbili zijazo nitaleta fursa tatu muhimu za kiuchumi, kaeni mkao wa kupokea, tupo pamoja,” alisema kupitia salamu fupi kwenye ukurasa wake wa Instagram
Kutangazwa kwa fursa hizo, ni moja kati ya juhudi nyingi zinazoendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya sita kupitia Mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali duniani.
Mpaka sasa, Tanzania imeweza kunufaika na uwekezaji pamoja na uuzaji wa bidhaa mbalimbali katika nchi tofauti tofauti, kazi nzuri ambayo imekuwa ikiratibiwa na Mabalozi.