November 15, 2024

CHINA, INDIA KUSHIRIKI MAONYESHO YA KIMATAIFA YA MADINI NA TEKNOLOJIA MKOANI GEITA

0

Na Prosper Makene,Geita
Takribani Mataifa nane yakiwemo mataifa yenye uchumi mkubwa Duniani ya China na India, yamekubali kushiriki katika maonesho ya saba ya madini na teknolojia ambayo yataanza kesho tarehe 2 Oktoba mpaka Oktoba 13 katika viwanja vya EPZA, Bomba Mbili mkoani Geita.
Mbali na wadau wakubwa kutoka nchini China na India, maonyesho hayo pia yatavutia mataifa mengine kutoka Afrika yakiwemo Afrika Kusini, Burundi, Rwanda, Kongo, Uganda na Kenya.
Maonyesho haya yameratibiwa mahususi katika kusaidia kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya madini nchini ambapo vile vile yanatarajiwa kushirikisha jumla ya washiriki zaidi ya 600 kutoka ndani ya nchi ambao wanajihusisha na bishara za mbalimbali ikiwemo biashara ya madini.
Vile vile, maonyesho haya yatayaleta kwa pamoja makampuni makubwa, ya kati na madogo kutoka ndani na nje ya nchi ambapo yatakutana kubadilishana ujuzi na teknolojia.
Akizungumza katika viwanja vya maonyesho haya mjini hapa leo kuhusu maandalizi kuelekea maonyesho haya yenye tija katika kukuza uchumi wa nchi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita (RAS) Mohamed Jumanne Gombati amesema Serikali imejipanga vilivyo kuhakikisha maonesho haya yanafanyika kwa weledi ili kuleta matokeo chanya.
“Maonyesho haya yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa wadau wa madini kutoka ndani na nje ya nchi, hasusani wachimbaji wetu wadogo na makampuni makubwa na madogo ambapo watajifunza na kuona teknolojia mpya ambazo zitaweza kuwasaidia kuleta mapinduzi katika sekta hii muhimu ya madini,” alisema.


Aidha, RAS Gombati alisema kuwa kwa mujibu wa ratiba ya maonyesho hayo ambayo yatadumu kuanzia kehso tarehe 2 Oktoba mpaka 13 Oktoba, kutakuwa na siku maalumu kwa shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuandaa siku maalum ya utalii wa madini, siku maalum kwa taasisi za fedha, makampuni ya bima pamoja na siku maalum kwa mifuko ya hifadhi ya jamii. .
“Tukio hili pia litakuwa na siku maalum kwa wazawa wa Geita ‘Wana Geita’ ambapo kwa pamoja watajadili fursa mbali mbali ambazo zipo mkoani hapa,” alisema.


Maonyesho hayo ya kimataifa ambayo yanaratibiwa na Serikali ya Mkoa wa Geita kwa kushirikiana na Wizara ya Madini na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Gombati alisema kuwa maonyesho hayo yatasaidia vilevile kutafsiri falsafa ya uchumi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 4r (maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoani Geita, Mhandisi Gabriel Robert alitoa wito kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo kutoka Geita na sehemu nyingine nchini kushiriki katika maonyesho haya adhimu ya madini na teknolojia ili kuweza kukuza wigo wa biashara zao.
“Maonyesho haya ya Kimataifa ya Madini na Teknolojia yatafungua pengo kubwa la maarifa (Knowledge Gap) kati ya wafanyabiashara, sio tu katika tasnia ya madini, lakini katika sekta nzima ya biashara nchini Tanzania,” alisema Mhandisi Robert Gabriel ambaye kwa nyakati tofauti ameshawahi kuwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Geita na Mara.


Alisema kuwa maonyesho haya yanatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kibiashara na vile vile yatafungua fursa za biashara kwa wafanyabiashara kubadilishana mawazo ya kibiashara, kukuza mahusiano pamoja na kupanua wigo wa masoko.
“Kwa mfano, maonyesho haya yatatoa fursa nyingi kwa wachuuzi wa chakula, na wafanyabiashara wengine wadogo wadopgo ambapo wataweza kuuza bidhaa zao bila shida,” aliongeza.
Alimalizia, “Naomba nimalizie kwa kumshukuru Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara nchini, Rais wetu amekuwa msikivu kwa kuweza kusikiliza matakwa ya wafanyabiashara na ameweza kuyafanyia kazi kwa kiasi kikubwa, kwa sababu hii sisi kama chemba ya wafanyabiashara Mkoani Geita tunamshukuru sana Rais wetu.”


Naye, mratibu wa Maonyesho hayo Charles Chacha ambaye vile vile ni Katibu Tawala Msaidizi (Viwanda Biashara na Uwekezaji) ametoa wito kwa wafanyabiashara kutoka katika sekta ya madini na maeneo mengine kuendelea kujisajili ili waweze kupata nafasi ya kushiriki katika maonyesho haya yenye tija kwa Mkoa na Taifa.
“Tunatarajia kuweza kuona zaidi ya watu elfu 20 wakijitokeza kuja kwenye maonyesho haya ya 7 ya Kimataifa ya Madini na Teknolojia,” alisema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page