November 15, 2024

HEKTA 2,871.782 KUTOLEWA KWA WANANCHI WA KISIWA CHA MAISOME

0

Na Mwandishi wetu -Bungeni Dodoma.

Serikali imeridhia ombi la Wananchi wa kisiwa cha maisome kupatiwa hekta 2,871.782 kwa ajili ya matumizi yao ya shughuli mbalimbali za kijamii.

Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mhe. Eric James Shigongo (Mb) aliyetaka kujua Serikali itatimiza lini ahadi ya kuwakatia eneo la hifadhi wananchi wa Kisiwa cha Maisome kwa kuwa idadi ya wakazi imeongezeka.

Aidha Mhe. Kitandula aliongeza kuwa Baraza la Mawaziri liliridhia jumla ya hekta 2,871.782 zimegwe kutoka kwenye hekta 12,191.02 za eneo la hifadhi, na hivyo kufanya hifadhi kubakiwa na hekta 9,319.238.

Vilevile Mhe. Kitandula aliongeza kuwa tayari Wizara imewasilisha rasimu ya Tangazo la Serikali (Notisi ya Kusudio la Kutangaza Mabadiliko ya Eneo la Msitu wa Hifadhi wa Taifa Maisome ya Mwaka 2024) kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwaajili ya upekuzi ili kukamilisha taratibu za kisheria za mabadiliko hayo.

Aidha, Mhe. Naibu waziri alilifahamisha bunge kuwa tayari Wizara imekamilisha zoezi la kupitia mpaka wa hifadhi na kupima upya eneo lililobaki; na tayari ramani mpya ya eneo hilo imeandaliwa. 

Mhe. Kitandula aliongeza kuwa kufuatia hitaji la wananchi wa eneo hilo kuruhusiwa kuokota kuni kavu kwa ajili ya matumizi yao, TFS imeridhia ombi lao na utaratibu maalum umewekwa ambapo wananchi wanaruhusiwa kuokota kuni katika hifadhi ya Maisome mara tatu (3) kwa mwezi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page