November 14, 2024

Jitihada Za WOWAP Kupambana Na Ukeketeji Zaanza Kuzaa Matunda

0

 NA MWANDISH WETU, Singida

SHIRIKA lisilokuwa la Kiserikali la Woman Wake Up (WOWAP) limesema kampeni mbalimbali zinazoendelea nchini zimeongeza uelewa wa wananchi juu ya madhara ya ukeketaji na hivyo kupunguza vitendo hivyo katika mkoa wa Singida.

Akizungumza kwenye mnada wa Njia panda ya Merya Halmashauri ya Singida Mratibu wa Wowap, Nasra Suleiman, amesema kumekuwa na muamko chanya, pamoja na ongezeko la uelewa wa madhara ya ukeketaji katika jamii nchini.

Alisema kuwa, Shirika la WOWAP limekuwa likifanya utekelezaji wa mradi wa kupinga vitendo vya ukeketaji, mradi muhimu unafadhiliwa  na Shirika la Woman Actions Against FGM (WAAF) la Japan.

Aidha, katika kutekeleza mradi huo, Nasra amesema wanatumia njia ya kufanya kampeni mbalimbali za kutokomeza ukeketaji wa wanawake na wasichana na kampeni hizo zinafanyika kwenye mikusanyiko mikubwa ya watu ikiwemo minadani.

“Mnada wa njia panda ya Merya unakusanya watu wengi, tumefika na kutoa elimu hapa ,mwitikio ni mkubwa nawengi waliuliza maswali hasa kuhusiana na suala la adhabu,” alisema

Aliongeza kuwa, sababu kubwa zinazopelekea ukeketaji ni baadhi ya jamii kushikilia mila na desturi mbaya, imani za dini potofu, kuhifadhi bikra, na mila potofu za kulinda heshima ya familia.

Alisema kuwa, katiba ya Tanzania inakataza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, vitendo ambavyo ni hatarishi, ikiwemo ukeketaji.

 “Mpango wa taifa wa utekelezaji wa kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na Watoto wa mwaka 2017- 2018/ 2021-2022  umeeleza kwa ufasaha kwamba ukeketaji ni mila inayoathiri wanawake na Watoto,” alisema

Walengwa wa mradi huo ni wanawake, watoto na jamii nzima kwa ujumla lengo ni kuhamasisha jamii iwe sehemu ya kusaidia na kulinda watoto wa kike  dhidi ya vitendo vya ukeketaji.

Ofisa Maendeleo ya jamii, Mkoa wa Singida, Shukrani Mbago, alisema wanaendelea kutoa elimu kwani wananchi wakielimika wataachana na mila ya ukeketaji.

Amelipongeza shirika la WOWAP kwa jitihada za dhati za kupambana na wimbi baya la ukeketeji dhidi ya wasichana kwa kutoa elimu kwa wananchi.

” Kwa kushirikiana na WOWAP, tumekuwa tukitoa elimu katika maeneo mbalimbali kwa wananchi ili waache vitendo vya ukeketaji, jamii inatakiwa ipewe elimu ya kutosha ili iweze kutokomeza mila hiyo,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page