JKCI: WATU ZAIDI YA 200 WAPIMWA MOYO KTK MAONESHO YA 7 YA MADINI GEITA
Na Prosper Makene
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Saleh Hamisi Mwinchete amesema kuwa watu zaidi ya 200 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati huu wa maonyesho ya saba ya kimataifa ya Teknolojia ya madini yanayoendelea mkoani Geita.
Maonesho hayo ambayo yameanza tarehe 2 Oktoba na kufunguliwa tarehe 5 Oktoba na Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko yatadumu kwa siku kumi mpaka Oktoba 13.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya EPZA Magogo mjini hapa, Dkt Mwinchete amesema kuwa JKCI imeamua kutoa fursa kwa wananchi wa Geita na mikoa ya jirani kupima magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na sukari kwenye damu katika kliniki maalum ambayo inafanywa na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Ameongeza kuwa watu wengi ambao wamepatiwa huduma katika banda la JKCI wamekutwa na magonjwa mbalimbali ya moyo ukiongozwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu.
“Wengi wa watu ambao tumeshawapatia huduma, wengi wao tumewakuta shinikizo la juu la damu. Watu wengi wanakuwa wanatembea wakiwa na matatizo ya presha bila wao kujua, tunawashauri watu wote kuja katika banda letu na kupatiwa matibabu ya vipimo bure,” alisema.
Alisisita: “Tunawashauri watu kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara, kufanya mazoezi, kula matunda na mboga za majani kwa wingi, pamoja na kupata usingizi wa kutosha ili kuweza kuwa na afya bora.”
Kwa upande wake Daktari kutoka kitengo cha moyo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato Liberius Libent amesifu ushirikiano waliongia na JKCI ambapo toka waanze ushirikiano huo mwaka 2022 wameshafanya upasuaji mdogo wa moyo kwa watu wane.
Amesema kuwa huduma za kibobezi kwa magonjwa ya moyo sasa zitakuwa zikipatikana katika hospitali ya Chato kwa ushirikiano na JKCI.
“Kila wiki ya tatu ya mwezi huwa tunapokea madaktari wa moyo kutoka hopsitali ya JKCI hatua ambayo imesogeza kwa ukaribu huduma za matibabu na vipimo karibu kwa watu wote wa kanda ya Ziwa na mikoa jirani,” alisema.
Mwisho