November 15, 2024

MAKAMU WA RAIS AKIHUTUBIA BUDAPEST SUMMIT

0

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
ametoa wito kwa mataifa kutambua umuhimu kuweka mkazo katika taasisi ya familia
ya kiutamaduni ili kuifanya kuwa kiini cha maendeleo ulimwenguni.



 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia kwa niaba ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Tano wa
Idadi ya Watu (5th Budapest Demographic Summit) unaofanyika Jijini Budapest nchini Hungary. Amesema inahitajika nguvu ya pamoja kimataifa
katika kuimarisha ustawi wa familia ikiwemo kuzingatia kanuni na desturi za
kiutamaduni pamoja na kuunga mkono mafundisho ya dini ambayo yanakuza maadili
ya familia na kulinda usalama na mwendelezo wa familia.

 


Pia
Makamu wa Rais ametoa wito kwa serikali ulimwenguni kutengeneza na kutekeleza
sera, programu na sheria zitakazohakikisha usalama na uendelevu wa familia.
Aidha ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushirikiana na Bara la Afrika
katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na ongezeko la idadi ya watu
zikiwemo uhitaji wa huduma za afya na elimu, ukosefu wa ajira, upungufu wa
chakula na uhamiaji haramu.

 

Akitoa
mfano wa Tanzania katika mkutano huo wenye kauli mbiu ya “Familia Msingi wa
Usalama” Makamu wa Rais amesema nchini Tanzania familia inatambuliwa kama
msingi imara na muhimu ambayo ni mwanzo wa ujenzi wa mtandao wa mahusiano ya
jamii nzima. Ameongeza kwamba Tanzania familia inahusisha muunganiko wa ndoa ya
watu wa jinsia mbili tofauti,watoto wao pamoja na ndugu au wategemezi wao ambapo
pamoja na mambo mengine, familia hutumika kuimarisha utaratibu na utulivu
katika jamii na pia husaidia katika uwezo 
wa kufanya maamuzi na utatuzi wa matatizo pamoja na utulivu wa kifedha,
utoaji wa elimu na huduma za afya kwa wanafamilia na malezi.

 

Makamu
wa Rais amesema pamoja na kuendelea kusisitiza na kuimarisha ustawi wa familia,
serikali ya Tanzania imeendelea kuwekeza katika kujenga uchumi na kuboresha
miundombinu ya kijamii kwa maendeleo ya watu ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya
maji, umeme, elimu pamoja na utoaji wa elimu bila malipo kuanzia ngazi ya awali
hadi sekondari. Ameongeza kwamba serikali imeongeza jitihada katika kuwavutia
vijana ambao ni idadi kubwa iliopo nchini kushiriki katika kilimo biashara kwa
kuanzisha programu maalum ya Jenga Kesho iliyobora (BBT).

 

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema sababu za
kiuchumi na migogoro zinazopelekea ongezeko la wahamiaji ndizo zinazopelekea athari
ya mienendo ya idadi ya watu Barani Afrika. Amesema Tanzania imekuwa ikihifadhi
wakimbizi zaidi ya laki nne kutoka mataifa Jirani ambao wamekua wakitafuta
amani na ustawi wa Maisha yao. Makamu wa Rais ametoa wito kwa kwa nchi na
mataifa kuiunga mkono Tanzania katika kuwahudumia wakimbizi ambapo uwepo wao
huongeza mahitaji kama vile ya ardhi, maji, huduma za kijamii na miundombinu.
Pia ametoa wito wa kuboresha usalama wa kitaifa na kikanda, kuzuia migogoro,
kuimarisha na kulinda amani pamoja na kuongeza juhudi katika kuzuia na
kupambana na ugaidi.

 

Vilevile Makamu wa Rais amesema Tanzania inathamini
ushirikiano  na Jamhuri ya Hungary katika
nyanja ya Elimu na kuinua ujuzi. Amesema serikali imedhamiria kuimarisha
uhusiano na nchi ya Hungary katika ukuzaji wa ujuzi kwa vijana, uwekezaji
hususani katika kilimo na biashara ya kilimo, uongezaji wa thamani, utengenezaji
wa bidhaa, utalii na teknolojia.

 

Mkutano
huo wa siku mbili unahudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo
Wakuu wa Nchi na
Serikali kutoka mataifa mbalimbali, Watunga Sera, Viongozi wa Taasisi na
Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa Dini na Wanataaluma.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page