November 14, 2024

MAZOEZI HUIMARISHA AFYA YA AKILI NA MWILI-DKT. MASSA.

0

 Na.Elimu ya Afya kwa Umma.

Jamii imeaswa kuwa na desturi ya kufanya mazoezi mara kwa mara kwani yana faida kubwa katika kuimarisha afya ya  akili na afya ya mwili hususan kuzuia magonjwa yasiyoambukiza.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 13,2023  Jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Dkt.Khalid Massa katika Utekelezaji wa Mpango wa Mazoezi na Afya ya Mwili kwa watumishi ndani ya Idara ya Kinga ambapo watumishi wa idara hiyo wamekuwa na mpango wa kufanya mazoezi kila Jumatano na Ijumaa katika uwanja wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Milembe.

“Tumeanza mazoezi haya ili kuhamasisha katika kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, mazoezi yana umuhimu sana si tu afya ya mwili bali afya afya ya akili na yanaongeza performance kubwa katika utendaji wa kazi”amesema.

Hivyo,amehimiza wananchi pamoja na watumishi kujenga mazoea ya kufanya mazoezi.

Kwa upande wao baadhi ya Watumishi walio chini ya Idara ya Kinga, Wizara ya Afya wamesema mazoezi hayo ni muhimu kuimarisha afya zao na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi.

“Muda mwingi sana tunatumia kukaa ofisini haya mazoezi yatasaidia kuimarisha afya zetu na utendaji wa kazi nawasihi tufanye mazoezi”amesema  Yinza Jaka .

“Ukifanya mazoezi viungo vinakuwa vyepesi na haupatwi na magonjwa kiurahisi ni muhimu sana kufanya mazoezi”amesema Catherine Gitige.

“Mazoezi ni kila kitu tujitahidi kuzuia tabia bwete maana ukifanya mazoezi  unaondoa msongo wa Mawazo,tunahamasisha kila aliyeko nyumbani kila mahali kufanya mazoezi “amesema Juliana Mshama.

Ikumbukwe kuwa Idara ya Kinga, Wizara ya Afya  imeanzisha Mpango kwa watumishi kufanya mazoezi mara mbili kwa wiki Jumatano na Ijumaa jioni mara baada ya saa za kazi kuanzia saa 9:30 hadi saa 11:00 jioni hiyo ni katika kuungana na mkakati endelevu wa Wizara ya Afya wa Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page