MIFUMO YA KIELEKTRONIKI KUBORESHA HUDUMA ZA SEKTA YA ARDHI- NDEJEMBI
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Wizara yake imeanzisha mifumo ya kielektroniki ya kusimamia sekta ya Ardhi ikiwemo e-Ardhi ili kutoa huduma bora kwa Watanzania.
Waziri Ndejembi amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya Mifumo inayosimamia Sekta ya Ardhi kwa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Oktoba 30, 2024 Dar es Salaam.
Wajumbe wa Kamati hiyo na Watendaji wa Wizara ya Ardhi Zanzibar wamefanya ziara maalum kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya mifumo ya TEHAMA ya Ardhi ya Tanzania Bara inavyofanya kazi katika kuwahudumia Wananchi.
“Mifumo hiyo ni muhimu sana kwani inasaidia kuondokana na migogoro ya Ardhi ikwemo kuuzwa kwa viwanja mara mbili pamoja na kubadilisha matumizi ya maeneo kiholela” Mhe. Ndejembi.
Aidha, ameongeza kuwa Wizara yake imeanzisha mfumo wa kidigiti wa e-Ardhi utakaotumika kwenye mikoa yote nchini ambapo kwa sasa mfumo huo umeanza kutumika katika mkoa wa Arusha huku mkoa wa Dodoma kazi ya kuhamisha taarifa za majalada ya umiliki wa ardhi kutoka nakala ngumu kwenda nakala laini za kielektroniki ikiendelea.
Naye Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali ameyaelezea mafunzo waliyopata kuhusiana na mifumo hiyo kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar.
Aidha, Mhe. Rahma amesema, kuwa hivi karibuni wanatarajia kuwanzisha Mfumo wa kusimamia Ardhi Zanzibar (LARIS) kwa ajili ya ukusanyi wa taarifa mbalimbali za Ardhi.
Mhe Waziri ameongeza kuwa, mafunzo hayo yatawasaidia Wajumbe wa Kamati na watendaji wa Wizara yake kuwandaa Mfumo bora wenyenye ufanisi zaidi.
Kwa upende wake Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Yahaya Rashid Abdallah amsema, kamati yake imejifunza na kuridhishwa na mfumo wa TEHAMA wa e-Ardhi (Tanzania Bara) na kusisitiza kuwa Mfumo wa LARIS (Zanzibar) utasaidia kuleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Ardhi kwa kutambua, kupanga, kupima na kumilikisha Ardhi kulingana na Mpango wa Matumizi bora ya Ardhi.