Mwenge Wa Uhuru Kuzindua Miradi Ya Maendeleo Singida
Na Danson Kaijage,Singida.
MKOA wa Singida unatarajia kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Tabora kesho tarehe 22.9.2023 katika viwanja vya Malendi wilayani Iramba ambao utapokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba.
Mwenge huo wa Uhuru unatarajia kuzunguka katika wilaya zote Saba Iramba, Mkalama, Singida DC, Singida MC, Ikungu, Itigi na Manyoni huku miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa inazinduliwa kwa faida ya Watanzania hususani wakazi wa Mkoa wa Singida.
Aidha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2033 utaambatana na kauli mbiu Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa Viumbe Hai, kwa Uchumi wa Taifa huku ukizindua miradi ya maendeleo pamoja na kuhamasisha amani upendo na utulivu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida zinaeleza kuwa maendeleo ambayo yanachochewa na Rais wa awamu ya Sita Dk. Samia Suluhu Hassan zinalenga kuwafanya watanzania kuishi uchumi wa kati.
Sambamba na hilo taarifa zinaeleza kuwa kwa Mkoa wa Singida kuna miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na uchimbaji wa mabwawa, miundombinu ya afya, maji, barabara, nishati nk.
Kutokana na hali hiyo wananchi wa Mkoa wa Singida wameshauriwa kuhakikisha wanalinda miundombinu ya miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inatekelezwa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia.
Aidha wananchi wa Mkoa wa Singida pamoja na halmashauri zote wameshauriwa kuhakikisha wanajitokeza wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ili kupata ujumbe wa Mbio hizo na kujivunia maendeleo yanayotekelezwa na Serikali