NAIBU WAZIRI KIKWETE APONGEZA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA TASAF MKOANI SIMIYU
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe Ridhiwani Kikwete ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Simiyu.
Mhe. Kikwete amezitaka halmashauri zote nchini zinazotekeleza miradi ya maendeleo hususani kwenye sekta ya huduma za jamii kujifunza kutoka Mkoa wa Simiyu ambao una mafanikio makubwa.
Naibu Waziri ameyasema hayo mjini Bariadi baada ya kupokea ripoti ya utelekezaji wa miradi ya TASAF katika Mkoa wa Simiyu ambao pia ni miongoni mwa mikoa mitano inayotekeleza kwa majaribio miradi ya kupunguza umasikini awamu ya nne- Tanzania Poverty Reduction Project (TPRP IV).
“Simiyu ni miongoni mwa mikoa ya mfano kwa utekelezaji na usimamizi mzuri wa miradi ya TASAF, nimeridhishwa sana na hatua kubwa iliyopigwa katika utelekezaji wa shughuli hizi ambazo zina lengo la kuondoa umasikini na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii,” amesema.
Aidha, Mhe. Kikwete amesisitiza umuhimu wa waratibu na wasimamizi wa miradi ya TASAF kuendelea na ufuatiliaji wa karibu wakati wote wa utekelezaji kwa lengo la kuhakikisha miradi yote inaendana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amesema serikali kupitia TASAF imesitisha uhawilishaji fedha kwa walengwa kwa njia ya mitandao ya simu na badala yake, zoezi hilo litafanyika kwa njia ya benki au mlengwa kupewa fedha mkononi.
“Kumekuwa na changamoto kadhaa kwenye uhawilishaji fedha kwa njia ya simu, sasa ili kuepukana na changamoto hizo kwa sasa, walengwa watapokea fedha hizo kwa njia ya benki au kuchukua moja kwa moja,” amesema Mhe Naibu Waziri.
. Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bwana Shedrack Mziray akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Mtaa ya Mbiti Kata ya Mhanga kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kuzungumza na wananchi wa mtaa huo mara baada ya kukagua nyumba ya Mtumishi wa zahanati ya Mbiti iliyojengwa kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TASAF kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa, Prisca Kayombo, Mratibu wa TASAF mkoa, Nyasilu Ndulu amesema jumla ya shilingi Bil. 9.24 zimepokelewa kwa ajili utekelezaji wa miradi hiyo.
“Hadi sasa kaisi cha shilingi Bil. 6.03 sawa na asilimia 65 ya fedha iliyopokelewa zimeshatumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali kama ya afya na elimu,” alisema.
Katika sekta ya afya TASAF imewezesha kujengwa kwa Zahanati 9, Nyumba 14, majengo ya wagonjwa wa nje (OPD) 2, jengo la upasuaji 1, jengo la kuhifadhia maiti 1, wodi za mama na mtoto 5 pamoja na maabara 1.
“Kwa upande wa sekta ya elimu tumeweza kujenga vyumba 60 vya madarasa, ofisi 27 za walimu, matundu ya vyoo 186, maktaba 1, nyumba za walimu 4, majengo ya utawala 4 vyumba vya maabara 8 na mabweni 11,” alisema.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiburudika na baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Mtaa wa Mbiti Kata ya Mhanga iliyopo katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu mara baada ya kukagua nyumba ya Mtumishi ya zahanati ya Mbiti iliyojengwa kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)