November 15, 2024

NAIBU WAZIRI KIKWETE: WATUMISHI WA UMMA JIEPUSHENI NA MIKOPO KAUSHA DAMU

0

NA.LUSUNGU HELELA-SIMIYU

 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Ridhiwani Kikwete (Mb) amewatahadharisha Watumishi wa Umma kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa maarufu kwa jina la ” Kausha Damu” huku akisisitiza kuwa mikopo ya aina hiyo imekuwa ikidhalilisha na kutweza utu wa Watumishi katika Jamii.


 



Mhe.Kikwete ametoa tahadhari hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Busega Mkoani Simiyu wakati akihitimisha ziara yake aliyoianza mapema wiki hii Mkoani Mara.


 


Amesema mikopo hiyo imewafanya baadhi ya watumishi wa umma kuathirika kisaikolojia na kushindwa kufika katika vituo vya kazi na hivyo kuathiri utoaji wa huduma bora kwa wananchi. 


 



Amefafanua kuwa mikopo hiyo ambayo huchukuliwa kwenye Taasisi za Kifedha zisizotambulika imekuwa na riba kubwa ambayo huwapelekea Watumishi wengi kushindwa kuwasilisha marejesho na hivyo kupelekea kuuzwa kwa nyumba au vitu vya thamani wanavyo vimiliki.


 


Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Kikwete amewataka Watumishi kuanza kutumia Mfumo mpya wa kieletroniki wa kukopa (e-loans) ulioanza kutumika kuanzia Septemba 1, 2023 ambao unamuwezesha Mtumishi wa Umma kuomba mkopo pasipo kufika kwenye Taasisi ya Kifedha au Tawi la Benki.


 



Amesema mfumo huo umeanzishwa na Ofisi ya Rais – UTUMISHI na Utawala Bora ili kumsaidia Mtumishi wa Umma kupata mikopo katika Taasisi za Kifedha zinazotambulika na Mwajiri ili kumuepusha Mtumishi kukopa sehemu ambazo humpeleka Mtumishi kunyang’anywa kadi ya Benki.


 


Aidha, Mhe.Kikwete amewataka watumishi hao kujenga nidhamu ya matumizi ya pesa wanazopata kwa ajili ya mustakabali wa maisha yao ya baadaye baada ya kustaafu.


 


Amewasihi kujiwekea malengo ya kujiandaa kustaafu kuanzia leo ili wasije kuwa wateja wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Kuendeleza Jamii ( TASAF ).


 


“Hakikisheni hata hela mnazozikopa mnafanya uwekezaji wa kimkakati kwa ajili ya kujitegemea kiuchumi katika siku za mbeleni” amesisitiza Mhe.Kikwete


 


Katika ziara hiyo Mhe.Kikwete mbali ya kuzungumza na watumishi wa umma katika mikoa ya Mara na Simiyu pia amekagua miradi mbalimbali 


inayotekelezwa na TASAF pamoja na kuzungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na TASAF.


 


 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page