November 15, 2024

NEMC Yawataka Wamiliki Wa Mabasi Nchini Kuzingatia Utunzaji Wa Mazingira

0


Na Mwandishi Wetu,  Dar es Salaam 

BARAZA 
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka
wamiliki wa mabasi kuzingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa
kuweka vyoo na vitenganishi taka kwenye mabasi yao wanapokuwa safarini.

 Agizo
hilo limetolewa na  Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Mafwenga
Gwamaka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukithiri
kwa uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na abiria kwenye mabasi pamoja
na namna sahihi ya kudhibiti uchafuzi huo.


Akizungumza
katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa NEMC Jijini Dar es
Salaam,  Mkurugenzi huyo mesema abiria wa mabasi wamekuwa chanzo kikubwa
cha uchafuzi wa mazingira kwa kutupa taka madirishani na kuchimba dawa
maporini  wakati wa safari ndefu, hali inayopelekea kuhatarisha maisha
yao pamoja na kuchafua mazingira, hasa vyanzo vya maji.

“Kumekuwa
na tabia ya abiria kutupa mabaki ya vyakula madirishani popote pale, au
kwenda haja kubwa na ndogo wakati wa safari ndefu barabarani, ikiwa ni
pamoja na maeneo ya hifadhi za misitu na  mbuga za wanyama,”
alisema.

Aidha,
amesema, maeneo ya hifadhi na barabara zote zinatakiwa kulindwa, na
hivyo sio nzuri i kuchafua mazingira ya maeneo hayo muhimu ya nchi.

Ameongeza
kuwa mabasi yote ya abiria yanayofanya safari ndefu yanapaswa
kuzingatia kanuni za utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa kuweka
vitenganishi vya taka kwenye mabasi, hali itakayosaidia kuepuka uchafuzi
wa mazingira.

Dkt.
Gwamaka amesisitiza kuwa uchafuzi aina hii una athari kubwa katika
mazingira kwani huibua magonjwa ya mlipuko, husababisha kuchafuliwa na
kuziba kwa  vyanzo vya maji, na pia  hupelekea mikondo ya maji kuziba,
kusababisha mchafuko wa hali ya hewa pamoja na kuharibu ikolojia ya
wanyama na mimea.

Amezitaka
Halmashauri kote nchini kwa kushirikiana na Chama Cha Wamiliki wa
Vyombo vya Usafirishaji ( TABOA) pamoja na LATRA kuhakikisha elimu ya
utunzaji wa mazingira inatolewa na kujenga vyoo maeneo husika ili
kuepukana na adha hiyo ya uchafuzi wa mazingira.

Katika
hatua nyingine, Dkt. Gwamaka amewataka wenye viwanda kuhakikisha
wanazingatia mpango wa kutunza mazingira kwenye maeneo yao ya kazi kwa
kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kuhifadhi taka za viwandani na
majumbani ili kutunza Mazingira.

Vilivile
ameitaka jamii kuwa na tabia ya kutenganisha taka za plastiki,
kielekroniki, chuma, karatatasi na mabaki ya vyakula kuanzia majumbani
ili kupunguza mzigo kwa Halmashauri wa ukusanyaji wa taka sababu taka ni
fursa zinarejerezwa na kutoa ajira pamoja na  malighafi nyingine za
viwandani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page