Rais wa Indonesia atua Tanzania kwa ziara maalumu
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAISI wa Indonesia, Joko Widodo amewasili nchini Tanzania kwa ajili ya ziara maalumu ya siku mbili.
Mapema leo (Agosti 22,2023) Rais Widodo aliwasili Jijini Dar es Salaam na kupokelewa na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu Magogoni.
Rais Widodo na Rais Samia watakuwa na mazungumzo ya faragha, na baadaye watakuwa na mazungumzo rasmi kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza kwa kifupi juu ya ziara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amesema kuwa ziara hiyo imelenga kufungua maeneo saba mapya ya ushirikiano yakiwamo katika sekta za afya, nishati na madini.
Maeneo mengine yatakayotiliwa saini hati ya makubaliano ya ushirikiano ni sekta za uchumi wa buluu, ushirikiano wa kimataifa, uhamiaji na biashara.
Dk Tax amesema pamoja na kushirikiana katika harakati za ukombozi, tangu kuanzishwa ushirikiano wa kidiplomasia pamekuwepo na mafanikio makubwa katika sekta ya uwekezaji na kilimo.
Amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2023, Indonesia imewekeza nchini miradi ipatayo mitano katika sekta za kilimo, uzalishaji wa viwandani na ujenzi.
Ameeleza kuwa mwaka 1996, Indonesia ilianzisha Kituo cha Mafunzo kwa Wakulima Vijijini (Farmers’ Agriculture and Rural Training Centre-FARTC), kilichopo Mikindo mkoani Morogoro.
‘’Kwa kuzingatia kuwa, Indonesia imepiga hatua kubwa katika kilimo cha zao la mchikichi kutokana na kuwa na mbegu bora ya zao hilo, pamoja na teknolojia ya kisasa, ziara hii itapanua wigo wa ushirikiano katika zao la mchikichi,’’ amesema.
Pamoja na hayo, ameeleza kuwa ushirikiano huo utawawezesha wakulima wa zao hilo kunufaika na mbegu bora ya mchikichi, na hivyo kuwajengea uwezo na kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula ambayo yana soko kubwa nchini na duniani.
Dk Tax amesema kuwa Tanzania na Indonesia zina uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria katika nyanja za kimataifa tangu wakati wa harakati za kujikomboa kutoka katika utawala wa kikoloni kama wanachama wa Umoja wa Nchi zisizofungamana na Upande Wowote (NonAligned Movement –NAM) hivyo, nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali ya kimataifa.