November 15, 2024

Raisi Samia Apangua Baraza la Mawaziri, Airudisha Nafasi ya Naibu Waziri Mkuu Baada Ya Miaka 30

0

By MWANDISHI WETU, 
 Dar es Salaam 
RAISI Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, ambapo pamoja na mabadiliko mengine, amemchagua Mhe. Dotto Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu, nafasi ambayo ilikuwepo katika safu ya uongozi nchini takribani miaka 30 iliyopita.

Nafasi ya Naibu Waziri Mkuu ilianzishwa mwaka 1994, na Raisi Mstaafu Ally Hassan Mwinyi, ambapo Marehemu Augustino Lyatonga Mrema alichaguliwa kwenye nafasi hiyo ya juu. Hata hivyo, nafasi hiyo haikudumu kwa muda mrefu.


Baada ya miaka 30 sasa kupita, katika mabadiliko ya Maraza la Mawaziri yaliyotangazwa leo, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuirejesha nafasi hiyo na kumkasimisha madaraka aliyekuwa Waziri wa Madini, Mhe. Dotto Biteko kushika wadhifa huo.

Licha ya madaraka hayo, Raisi pia amemchagua Dkt. Biteko kuwa Waziri mpya wa Nishati, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Mhe. January Makamba. 

Aidha, katika mabadiliko hayo muhimu, Raisi Dkt. Samia ameamua kuifuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kuanzisha Wizara mbili zinazojitegemea, Wizara ya Ujenzi, na Wizara ya Uchukuzi.

Wakati Profesa Makame Mbarawa (aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi) ameteuliwa kuwa Waziri wa Wizara mpya ya Uchukuzi,  aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa sasa ni Waziri wa Ujenzi.

Mhe. January Makamba ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  kumridhi Dkt. Stagomena Tax ambae kwa sasa atasimamia Wizara ya Ulinzi.

Katika mabadiliko zaidi, Mhe. Omary Mchengerwa, (aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii) ameteuliwa kuwa Waziri mpya wa Ofisi ya Rais (TAMISEMI), huku Mhe. Angella Kairuki akichaguliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii. 

Dkt. Damas Ndumbaro (aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria) sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, huku Dkt. Pindi Chana akihamishiwa kwenye Wizara ya Katiba na Sheria. 

Mhe. Anthony Mavunde, aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, ameteuliwa kuwa Waziri wa Madini, huku Ndugu Jerry Slaa akichaguliwa kuwa Waziri mpya wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuirithi nafasi ya Mhe. Angelina Mabula.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page