November 15, 2024

Ujenzi wa kiwanda cha kusindika bangi katika Wilaya ya Musanze, nchini Rwanda umefikia asilimia 70% hadi sasa huku mradi huo ukitarajiwa kukamilika mwezi septemba mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa KKOG Rwanda, Rene Joseph ameliambia gazeti la New Times la Rwanda na kuongeza kuwa ujenzi huo umechelewa kutokana na changamoto ya miundombinu ya barabara.

Machi 2024, Serikali ya Rwanda ilitoa leseni ya miaka 5 ya kulima bangi kwa madhumuni ya dawa, uchimbaji na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za dawa kwa kampuni ya King Kong Organics (KKOG-Rwanda) inayoshirikiana na Shirika la Marekani la KKOG GLOBAL ambalo dhamira yake ni kuwa kinara wa soko katika kilimo cha bangi ya matibabu katika Bara la Afrika.

Bodi ya maendeleo nchini humo (RDB) imetenga eneo la hekta 35 katika Wilaya ya Musanze kwa Wawekezaji watano ambao wameonesha nia ya kuzalisha bangi ambapo pia Serikali ya Nchi hiyo pia imejitolea kutoa miundombinu kama vile barabara, umeme, uzio wa maeneo ya kilimo, kamera za uchunguzi ili kuzuia bangi kuingia mtaani kwa Wananchi.

Katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB) ilitenga fransi za Rwanda (Rwf) milioni 700 (Tsh. bilioni 1,428,000,000) kwa mradi wa kilimo cha bangi ambapo kwa mwaka 2024/2025, bajeti iliongezwa hadi kufikia fransi za Rwanda (Rwf) bilioni 2 (Tsh. bilioni 4,080,000,000) ambapo hekta 1 ya bangi inatarajiwa kuzalisha hadi dola milioni 10.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page