November 14, 2024

Serikali Yajizatiti Kupambana Dhidi Ya Biashara Haramu Ya Wanyamapori Na Mazao Ya Misitu

0

  Na Mwandishi Wetu, Mwanza


Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema tatizo la  ujangili na biashara haramu ya nyara za wanyamapori na mazao ya misitu imekuwa  ikiathiri ustawi wa jamii na kudumaza uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa hivyo ushirikiano dhidi ya vita  hiyo hauepukiki.

 Mwakilishi wa  Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Bw. Kiza Y. Baraga ametoa kauli hiyo  leo Jumatano Agosti 23, 2023 Jijini Mwanza  wakati akifungua  Warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi na watendaji wa vikundi vya uratibu wa doria kanda za  kiikolojia  (Task Coordination Groups- TCGs) dhidi ya ujangili na biashara haramu ya wanyamapori. 




Amesema ushirikiano katika kuishinda vita hiyo ni muhimu  kwani mitandao ya ujangili na usafirishaji haramu wa nyara za serikali  hupangwa nje ya hifadhi (mijini) na kutekelezwa ndani ya maeneo ya hifadhi ambapo ndipo zilipo rasilimali na hatimaye husafirishwa nje ya nchi kwenye masoko haramu.

Amesema Ujangili umekuwa ukiharibu sifa nzuri ya Tanzania hasa pale nyara na  mazao ya misitu yanapokamatwa nje ya mipaka ya nchi, hivyo mafunzo hayo ni muhimu katika kuwajengea uwezo watendaji katika kukabiliana na changamoto hiyo. 

Kufuatia hatua hiyo, Serikali imeanza kuzijengea uwezo mpana Taasisi mbalimbali zinazohusika katika  kukabiliana na changamoto za ujangili na biashara haramu ya wanyamapori na mazao ya misitu katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuhakikisha majangili wanakamatwa kabla hawajatekeleza ujangili ndani ya maeneo ya Hifadhi

Amezitaja Taasisi hizo ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za himasheria, pamoja na watendaji wa Idara na taasisi mbalimbali zinazohusiana na ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori na misitu. 

“Mitandao hii ya ujangili inahusisha wahalifu wa ngazi mbalimbali na hufadhiliwa na watu wenye uwezo mkubwa kifedha. Mafanikio ya kudhibiti  mitandao hii inategemea sana uwezo wa himasheria (Law enforcement) katika kanda zote  za Kiikoloji,” amesema Baraga 

Aidha, Baraga  amesema Wizara imeendelea kutekeleza jitihada mbalimbali za kuhakikisha  rasilimali za wanyamapori na mazao ya misitu nchini zinalindwa ipasavyo ikiwemo kubadili mfumo wa utendaji kazi wa taasisi za uhifadhi kutoka wa kiraia na kuwa wa kijeshi.

“Tumefanikiwa pia kuanzisha Kikosi Kazi Taifa Dhidi ya Ujangili “National Task Force Anti-poacting (NTAP), na Tasking and Coordination Groups (TCGs) ambavyo vinahusisha vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi za himasheria ili kuimarisha vita dhidi ya mitandao mikubwa ya ujangili,” Bw Kiza Baraga amesisitiza  


Ameongeza kuwa, Makosa ya biashara haramu ya nyara na mazao ya misitu ni ya kupangwa na yanavuka mipaka, Wizara imekuwa ikizishirikisha  Mamlaka mbalimbali katika kukabiliana na aina hiyo ya uhalifu ili kuweza kufikia malengo ya Wizara ya kutokuwa na matukio ya ujangili nchini ifikapo 2033.

“Navishukuru vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za himasheria, na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo UNDP kwa namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika vita dhidi ya ujangili wa wanyamapori na mazao ya misitu kwani ushirikiano huu umesaidia kupunguza ujangili kwa kiwango kikubwa,” amesema Bw. Kiza.

 Pia,  ametumia fursa hiyo kuwasihi   wajumbe kushiriki kikamilifu kwenye warsha hiyo ili kuongeza weledi na ujuzi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao adhimu ya kulinda rasilimali za nchi.  

Naye Meneja wa Mradi wa kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara za Wanyamapori. (IWT- Project ), Bw. Theotimos Rwegasira amesema katika kukabiliana na masuala ya ujangili hapa nchini Serikali ’ilizindua Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ujangili nchini  (2014-2019) kwa alengo muhimu la kudhibiti ujangili. 

“Serikali ilitafuta wadau kushirikiana nao katika kutekeleza mkakati huo mmoja wa wadau hawa ilikuwa ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP.’’ 


 Kwa kushirikiana na UNDP Wizara ya maliasili na Utalii inatekeleza Mradi wa Kupambana na Ujangili na biahashara haramu ya wanyamapori kwa njia shirikishi.

 Mradi huu ni wa miaka sita (2020- 2026) ambao lengo lake ni kusaidia juhudi za Serikali za kukabiliana na ujangili. 
 Amesisitiza kuwa kupitia utekelezaji wa Mradi huu tayari Wizara imebainisha mahitaji ya NTAP na TCGs na kuandaa mpango wa kuzijengea uwezo. 

Warsha hiyo  imeandaliwaa na Wizara ya Maliasili Utalii kupitia Mradi wa IWT. Aidha, warsha hii ni muendelezo wa mpango wa kuzijengea uwezo Taasisi za hima sheria ili kukabiriana na ujangili nchini hususan kikosi kazi cha Taifa cha kupambana na ujangili (NTAP) na Kanda za Kiikolojia za uratibu wa doria (TCG’s).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page