November 14, 2024

TAEC Watoa Kauli Nzito Biashara Ya Vyuma Chakavu

0

 NA MWANDISHI WETU,  Dodoma 


Wakati biashara ya ukusanyaji, uuzaji na uchakataji wa vyuma chakavu ikiendelea kushamiri kwa kasi nchini Tanzania, tahadhari imetolewa namna biashara hiyo inavyohatarisha usalama nchini, lakini pia kuathiri afya za watanzania na mazingira.

Kwa sasa biashara ya vyuma chakavu inaajiri maelfu na mamilioni ya watanzania kote nchini, ikiwemo watoto, ambapo inawawezesha kujikwamua kiuchumi na kujikimu katika mahitaji yao mihimu kwa njia ya kuokota na kuuza vyuma hivyo.


Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina zaidi ya Makampuni 106 yanayohusika na biashara ya kununua, kusafirisha na  kurejeleza vyuma chakavu kwa lengo la kutengeneza vifaa mbalimbali, ikiwemo vipuli vya vyombo vya usafiri,  mashine na vifaa vya ujenzi.

Makampuni hayo yaliyosajiliwa na Serikali kwa ajili ya biashara hiyo, yanachangia pato la Taifa ( kwa njia ya kodi na tozo), kwa kiasi kikubwa kutokana na ukubwa wa sekta hiyo nchini.

Licha ya umuhimu wake kiuchumi, biashara ya vyuma chakavu kwa kiasi kikubwa imeonekana kufanya vyema katika kusaidia harakati za kuboresha mazingira nchini.
Pamoja na umuhimu wa biashara hiyo, Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) leo imetoa tahadhari muhimu juu ya madhara makubwa ya biashara hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Lazaro Busagala, baadhi ya vyuma chakavu vinavyookotwa, kuuzwa na kurejezwa katika matumizi vina viambata vya mionzi mikali ya kiatomiki.

“Tunapenda kutoa tahadhari kwa Makampuni na watanzania wote wanaojihusisha na biashara ya vyuma chakavu kutumia tume yetu kwa ajili ya kupima usalama wa vyuma hivyo kabla ya matumizi yeyote,” aliagiza.


Amesema, uzoefu katika nchi mbalimbali unaonyesha kutokea kwa milipuko hatarishi kutokana na uuzwaji wa vyuma chakavu vyenye mionzi ya kiatomiki. 

“Hebu fikiri, ni hatari kiasi gani pale vipuli vya magari, ama nondo za kujengea nyumba na maofisi vikitengenezwa na vyuma vyenye mionzi ya kiatomiki inayoweza kusababisha mlipuko muda wowote,” Profesa Busagala alieleza.

Aidha, amesema kumekuwa pia na matukio ya uingizwaji haramu wa vyanzo vya mionzi hatarishi, ikiwa ni pamoja na madini ya Urani (Uranium) hali ambayo inahatarisha usalama wa nchi.


“Mpaka sasa kumekuwa na matukio takribani 17 ya uingizaji wa vyanzo vya mionzi mikali, pamoja na madini mengine hatarishi kwa njiia ya magendo,” alifafanua.

Akitoa mfano hai, amesema mnamo mwezi September 6 2012, TAEC kwa kushirikiana na Taasisi nyingine walifanikiwa kumkamata mtanzania mmoja Jijini Dar es Salaam ambaye aliingiza nchini kinyemela kilogram 9 za madini ya Urani yaliyochakatwa.

“Urani ni madini yenye madhara makubwa sana endapo tahadhari haitachukuliwa katika swala zima la matumizi yake, haswa katika udhibiti,” alieleza.

Malick Meshak, mmoja kati ya wafanyabiashara wa vyuma chakavu Jijini Dodoma, amesema tahadhari hiyo ni ya umuhimu sana, na imekuja wakati muafaka kwani biashara hiyo inakuwa kwa kasi kubwa sana hapa nchini.


“Kimsingi, biashara ya vyuma chakavu ina faida sana kwa Taifa, lakini katika kusaidia kuwakwamua  watanzania wanyonge kiuchumi, kinachotakiwa ni kuwekwa kwa miongozo na kanuni thabiti za kusimamia sekta hii,” alisema.

Raphael Chilanzi, mnunuzi wa vyuma chakavu katika eneo la Chang’ombe Jijini Dodoma amesema ukusanyaji wa vyuma chakavu ni sekta inayohitaji umakini na ufahamu wa hali ya juu, tofauti kabisa na hali ilivyo kwa sasa.


” Wengi wanao okota vyuma chakavu hawana elimu yeyote ya maswala ya utaalamu wa vyuma, wanaweza okota hata bomu, au kifaa chochote hatarishi kwani akili yao inawaza kupata fedha tu,” alieleza.

Pamoja na tahadhari nzuri iliyotolewa, ameiomba TAEC kuangalia uwezekano wa kushirikiana na Serikali za mitaa kuwatambua watanzania wanaojihusisha na biashara hiyo ili kuwapatia mafunzo maalumu.

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC)  ni Taasisi ya Serikali inayosimamia na kuratibu masuala yote yanayohusu mionzi hapa nchini ikiwa na maabara ya kisasa ambayo ni mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You cannot copy content of this page