Tanzania Inatarajia Kuvutia Watalii Wa Kigeni Milioni 5 ifikapo 2025
Na Mwandishi Wetu, Arusha
TANZANIA inatarajia kuvutia watalii wa kigeni wapatao milioni 5 nchini ifikapo mwaka 2025, idadi kubwa zaidi ya lengo lililowekwa na Wizara ya Maliasili na Utalii la kuhakikisha nchi inapokea angalau watalii milioni 4.5 miaka miwili ijayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa alielezea matarajio hayo mazuri Jijini Arusha wakati akishuhudia tukio la kihistoria la uhamiaji wa nyumbu wakubwa, safari ya kilomita 800 ya kundi kubwa la nyumbu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Alieleza kuwa, tukio la uhamaji wa nyumbu kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kutafuta malisho safi na mabichi kupitia Mto Mara, limekuwa likiwavutia mamilioni ya watalii kutoka nchi mbalimbali kwa takribani miaka 60 sasa.
“Hili ni moja kati ya matukio muhimu ambayo yanaipa sekta ya utalii nchini Tanzania heshima kubwa, ” alieleza.
Aidha, Waziri Mchengerwa amesema wizara itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kwa lengo la kuboresha mazingira ya utalii wa aina zote hapa nchini ili kuwavutia watalii wengi zaidi kuja nchini.
Sekta ya utalii inachangia angalau asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni nchini Tanzania.