TARURA IMEJIPANGA KUBORESHA MTANDAO WA BARABARA
Arusha
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) imejipanga kuboresha mtandao wake wa barabara kwa kuziwekea lami na nyingine changarawe kwa viwango ambavyo zitadumu kwa muda mrefu kutokana na bajeti ya wakala huo kuongezeka zaidi ya mara tatu.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Wakala huo Mhandisi Florian Kabaka wakati akiongea na waandishi wa habari katika maonesho yanayoendelea viwanja vya AICC jijini Arusha kwenye kikao kazi cha Wenyeviti na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa hazina.
“TARURA tutaendelea kujenga barabara kwa nguvu zaidi kwani katika miaka mitatu hii kiwango cha bajeti kimepanda zaidi ya mara tatu na hii inatuwezesha kuwa na uwezo wa kuhudumia barabara zetu kwa ubora.Tunamshukuru sana Mhe. Dkt. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea bajeti kila mwaka.
Amesema kutokana na ongezeko la bajeti hiyo wameweka mipango ya kuboresha mtandao wa barabara kila mwaka kwa kuingiza barabara za changarawe kuwa katika kiwango cha lami pia barabara za udongo kuwa kiwango cha changarawe zenye ubora.
Kwa upande wa maabara ya TARURA, Mhandisi Kabaka ameongeza kusema kwamba itaendelea kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa yenye viwango na ubora kwa kupima malighafi zote zinazohusika katika ujenzi wa miundombinu kabla ya kuanza ujenzi na matengenezo ili kuepuka ujenzi wa viwango vya chini.
Naye, Mhandisi Mshauri Pharles Ngeleja kutoka TARURA Makao Makuu amesema mtandao wa barabara wa Wakala huo ni mkubwa sana hivyo wameamua kutumia teknolojia mbadala ili kuweza kufungua barabara nchi nzima ndani ya kipindi kifupi.
Amesema hadi sasa wameweza kujenga barabara za teknolojia mbadala Km. 28 ambazo zimejengwa katika mikoa ya Mwanza, Kigoma, Rukwa pamoja na Morogoro na bado wanaendelea kujenga maeneo yote ambayo rasilimali inapatikana eneo husika.
Kwa upande wa madaraja amesema tayari wanajenga madaraja kwa kutumia mawe na madaraja hayo ni imara na hivyo kuwafungulia wananchi kuweza kutumia na kuwarahisishia kupata huduma mbalimbali muhimu kwenye maeneo yao pamoja na kuwafungulia uchumi kwa kufika kiurahisi kwenye masoko.