UZINDUZI WA MRADI WA UBORESHAJI WA HUDUMA YA MAMA NA MTOTO ULIOWASHIRIKISHA WATAALAM KUTOKA WIZARA YA AFYA TANZANIA,ZANZIBAR,TAMISEMI,NA WAWAKILISHI WA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI
Na Peter Mkwavila DODOMA
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la CMSR-Tanzania lenye makao yake makuu Dodoma kwa kushirikiana na Wizara ya afya ya Tanzania bara na Zanzibar limedhamiria kusaidia uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto kwa kununua vifaa tiba. muhimu ambavyo vitakakavyotumika kuwahudumia watoto wachanga na akina mama katika kipindi cha ujauzito na wakati wa kujifungua.
Aidha, shirika hilo litasaidia kutoa mafunzo kwa watoa huduma za mama na mtoto ili kuwajengea uwezo wataalam hao,katika mradi huu unaojulikana kwa jina la IMaNHC (Improving Maternal and Neonatal Health Care) unalenga kupunguza vifo vya watoto wachanga na akina mama na vile vitokanavyo na matatizo ya uzazi.
Afisa huyo wa mradi pia alisema, mbali na ununuzi wa vifaa, shirika litawajengea uwezo madaktari na wauguzi wanaotoa huduma za mama na mtoto kwenye wodi za watoto wachanga, kliniki ya waja wazito na wanapojifungua.
Hayo yamesemwa na Meneja msaidizi wa mradi huo Dk. Hamoud Ndenge alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha uzinduzi wa mradi huo uliowashirikisha wawakilishi kutoka Wizara za afya Tanzania bara na Visiwani, TAMISEMI, na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya CUAMM, COPE, AVSI, na AICS uliofanyika jijini Dodoma.
Dk Ndenge alisema kuwa uzinduzi wa mradi huo unafuatia kikao cha pamoja cha Wizara husika na wadau wa nchi hizi tatu kilichofanyika jijini Nairobi mwezi Juni 2023.
Alisema kuwa vifaa vitakavyonunuliwa vitawezesha kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma ya mama na mtoto inayotolewa katika vituo vilivyo kwenye mradi huo kulingana na aina na idadi ya vifaa kwa kila kituo imetokana na tathmini ya pamoja iliyofanywa na timu ya wataalamu wa afya ya mama na mtoto wa Wizara ya afya na TAMISEMI pamoja na CMSR-Tanzania.
Alisema kuwa mradi huu pia unashirikisha nchi za Kenya na Uganda kwa lengo la kuanzisha ushirikiano wa masuala yanayohusu afya kwa ujumla na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wataalam katika nchi hizi tatu za Afrika Mashariki.
Alisema kuwa kwa Tanzania bara tayari vituo vinne vimeshirikishwa kwenye mradi huo ambavyo ni pamoja na Hospitali ya St. Gemma na vituo vya afya vya Makole, Hombolo na Mkonze vyote vikiwa katika Halmashauri ya jiji la Dodoma. Kwa upande Zanzibar vituo vitano vimeshirikishwa ikiwemo Hospitali moja na vituo vya afya vinne.
Afisa Msaidizi wa mradi wa uboreshaji wa huduma za mama na Mtoto, (Improving Merernal and Neonatal Health care) (IMANHC) Dkt Hamoud Ndenge akizungumza kwenye uzinduzi na wadau walioshirikishwa likiwemo Shirika la Centro Salute Globale,Centro Mondiauta Sviuppo Reciproco,Doctors With Africa Cuamm na Cooperazione Paesi Emergenti (COPE) uliofanyika Dodoma.
Aidha, Dk. Ndenge alifahamisha kuwa mradi huu ulitambulishwa katika ngazi za wizara ya Afya Tanzania bara na Zanzibar,TAMISEMI, Mkoa na Halmashauri husika na umepokelewa kwa mtizamo chanya wa kufikia malengo tarajiwa.