WANANCHI KIJIJI CHA NGAHOKORA KUNUFAIKA NA NISHATI YA UMEME
Na Mwandishi wetu- RUVUMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha linafikisha huduma ya umeme katika Kijiji cha Ngahokora kufikia mwezi Desemba mwaka huu.
Mhe. Jenista ametoa agizo hilo mara baada ya kuzindua madarasa ya mfano ya Elimu ya Awali katika Shule ya Msingi Ngahokora iliyopo Kata ya Kizuka, Kijiji cha Ngahokora , Wilaya ya Songea Vijijini ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma.
Ameeleza kuwa kufikishwa huduma hiyo muhimu itakuwa mkombozi kwa wakazi wa eneo hilo katika kujikwamua kiuchumi kwa sababu utasaidia katika shughuli za uzalishaji na matumizi ya nyumbani pamoja kusaidia katika huduma za afya pindi wananchi wanapoenda kupatiwa matibabu katika Zahanati na Vituo vya afya.
“Ilani ya Chama Cha Mapundizi (CCM) tunaitekeleza kwa miaka mitano na ndani ya mwaka wa pili na sasa tunamalizia wa tatu mwaka 2021 umeme umefika Magagula kisha ukaelekea Kizuka na 2023 umeme utaelekea Mbilo na kisha hapa Ngahokora kwa sababu kama Serikali tunatambua umuhimu wa nishati hii muhimu katika maendeleo kuanzia ngazi ya familia na Taifa,” Ameeleza Mhe. Jenista.
Pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga hospitali ya Wilaya iliyopo eneo la Mpitimbi ambapo zaidi ya Bilioni mbili zimewekezwa katika ujenzi wa hospitali hiyo na kutoa wito kwa wananchi kuitumia kupata huduma.
“Wananchi wa Ngahokora nyie ni sehemu ya wanufaika wa ile hospitali ya Wilaya ya Mpitimbi zaidi ya Bilioni mbili zimewekezwa pale kwani itawasaidia msitembee umbali mrefu kutafuta matibabu kutoka hapa Ngahokora ni rahisi kufika hospitali ya Mpitimbi kuliko kwenda Peramiho na niliwaahidi kutoa fedha ili kuunganisha barabara itakayoasaidia kufika kwa urahisi hapo Mpitimbi,” Amefafanua Waziri huyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Bw. Menas Komba amebainisha kwamba kijiji hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo barabara, maji, uhaba wa vitanda vya kujifungulia kwa kina mama , umeme pamoja na mawasiliano lakini Serikali imeendelea kuzitatua kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu na kufanya shughuli za uzalishaji.
Aidha Diwani wa Kata ya Kizuka Mhe. Jacob Nditi amebainisha kwamba utekelezwaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayofanywa na Serikali katika Kijiji hicho inaonyesha nia njema ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwaletea wananchi wake maendeleo na mabadiliko ya kiuchumi.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ngahokora Bi. Tumaini Kaaya ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundo mbinu ya elimu akisema kuwa kukamilika kwa madarasa hayo kutatoa mwamko kwa wazazi kupeleka watoto shule na wanafunzi kujifunza katika mazingira rafiki.
“Tunaishukuru serikali kwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika kijiji chetu, Mhe. Mbunge kwa kutupatia madarasa mawili ya mfano ya elimu ya awali, madarasa mawili ya shule ya msingi Ngahokora, tunaishukuru TARURA kwa kuanza kuondoa visiki ili kuchonga barabara na TANESCO kutuongeza nguzo 53 ili kutuletea huduma ya umeme,” Ameshukuru Afisa huyo.
Nao baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Msingi Ngahokora wakisoma risala yao wameeleza kwamba kujengwa kwa madarasa hayo kwao ni chachu kubwa ya kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao huku wakimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya elimu.