WAZIRI MKUU AIPONGEZA TARURA KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA MAWE KWENYE UJENZI WA MADARAJA NA BARABARA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kutumia teknolojia ya mawe kwenye ujenzi wa madaraja na barabara nchini.
Waziri Mkuu ameyasema hayo alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wahandisi yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani city jijini Dar es Salaam.
“Najua wahandisi mna changamto nyingi lakini pamoja na changamoto hizo bado najua adhma yenu ni nzuri, lengo ni kujiweka pamoja ili muweze pia kushiriki kwa kina kwenye miradi yetu, nilipopita hapo kwenye banda la TARURA, wameonyesha jambo moja zuri sana, kwamba kwasasa wanajenga barabara zetu kwa kutumia malighafi zilizopo maeneo husika, nilifanya ziara mkoani Singida katika Wilaya ya Mkalama ambapo nilizindua daraja kwenye barabara moja kati ya barabara za vijijijini iliyojengwa na TARURA kwatumia teknolojia rahisi na malighafi zilizopo eneo la palepale kijijini”.
“Niliona daraja zuri la mawe ambalo Lori la tani 40 lilikuwa linapita, pia wamejenga madaraja mengine mengi baada ya kuagiza teknolojia hii itumike na leo nimeona madaraja mengi ya mawe yamejengwa na hivi karibuni nitafanya ziara mkoani Iringa nikaone daraja refu la mawe ambalo limejengwa, haya ni mafaniko makubwa”, amesema Mhe. Waziri Mkuu
Naye, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff amesema moja ya vipaumbele ni kutumia teknolojia mbadala kwaajili ya kupunguza gharama, kuongeza ufanisi wa kazi kwa maana ya kupunguza muda wa utendaji kazi, lakini vile vile kulinda mazingira pamoja na usalama wa watumia barabara na pia kupandisha hadhi barabara mfano kutoka changarawe kwenda lami au kutoka udongo kwenda changarawe.